Genesis 20

Ibrahimu Na Abimeleki

1 aBasi Ibrahimu akaendelea mbele kutoka huko hadi nchi ya Negebu na akaishi kati ya Kadeshi na Shuri. Kwa muda mfupi alikaa Gerari kama mgeni, 2 bhuko Ibrahimu akasema kuhusu Sara mkewe, “Huyu ni dada yangu.” Kisha Abimeleki mfalme wa Gerari akatuma Sara aletwe, naye akamchukua.

3 cLakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto wakati wa usiku na kumwambia, “Wewe ni kama mfu kwa sababu ya huyu mwanamke uliyemchukua; yeye ni mke wa mtu.”

4 dWakati huo Abimeleki alikuwa bado hajamsogelea, kwa hiyo akasema, “Je, Bwana utaliharibu taifa lisilo na hatia? 5 eHakusema kwangu, ‘Huyu ni dada yangu,’ naye Sara pia hakusema, ‘Huyu ni kaka yangu’? Nimefanya haya kwa dhamiri njema na mikono safi.”

6 fKisha Mungu akamwambia katika ndoto, “Ndiyo, najua ya kwamba umefanya haya kwa dhamiri safi, kwa hiyo nimekuzuia usinitende dhambi. Ndiyo sababu sikukuacha umguse. 7 gSasa umrudishe huyo mke wa mtu, kwa maana ni nabii, naye atakuombea nawe utaishi. Lakini kama hutamrudisha, ujue kwa hakika kuwa wewe na watu wako wote mtakufa.”

8Kesho yake asubuhi na mapema Abimeleki akawaita maafisa wake wote, na baada ya kuwaambia yote yaliyotokea, waliogopa sana. 9 hKisha Abimeleki akamwita Ibrahimu na kumwambia, “Wewe umetufanyia nini? Nimekukosea nini hata ukaleta hatia kubwa namna hii juu yangu na ufalme wangu? Umenifanyia mambo ambayo hayakupasa kufanyika.” 10Abimeleki akamuuliza Ibrahimu, “Ulikuwa na kusudi gani kufanya hivi?”

11 iIbrahimu akajibu, “Niliwaza kwamba, ‘Hakika hakuna hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa sababu ya mke wangu.’ 12 jPamoja na hayo, ni kweli kwamba yeye ni dada yangu, binti wa baba yangu ingawa si mtoto wa mama yangu; basi akawa mke wangu. 13 kWakati Bwana aliponifanya nisafiri mbali na nyumbani mwa baba yangu, nilimwambia, ‘Hivi ndivyo utakavyoonyesha pendo lako kwangu: Kila mahali tutakapokwenda, kuhusu mimi sema, “Huyu ni kaka yangu.” ’ ”

14 lKisha Abimeleki akatwaa kondoo na ng’ombe, na watumwa wa kiume na wa kike akampa Ibrahimu, akamrudisha Sara kwa mumewe. 15 mAbimeleki akasema, “Nchi yangu iko mbele yako, ishi popote unapotaka.”

16Akamwambia Sara, “Ninampa kaka yako shekeli elfu moja za fedha. Hii ni kufidia kosa lililofanyika dhidi yako mbele ya wote walio pamoja nawe; haki yako imethibitishwa kabisa.”

17 nKisha Ibrahimu akamwomba Mungu, naye Mungu akamponya Abimeleki, mke wake, na watumwa wake wa kike kwamba waweze kupata watoto tena, 18 okwa kuwa Bwana alikuwa ameyafunga matumbo ya wote katika nyumba ya Abimeleki kwa sababu ya Sara, mke wa Ibrahimu.
Copyright information for SwhKC